Mzee Majuto afariki dunia,.Muhimbili watoa maelezo.

Msanii mkongwe wa vichekesho Amri Athuman’ King Majuto’ amefariki dunia usiku huu baada ya kulazwa siku chache zilizopita katika hospitali ya Muhimbili jijini Dar es salaam.
Mchekeshaji Joti ndio wa kwanza kutoa taarifa hizo kupitia mtandao wa instagram.
“R.I.P @Kingmajuto Umetuachia Maumivu Makubwa sana ktk Tasnia ya Comedy Tanzania Sisi wanao,Tutakukumbuka kwa kazi zako,Upendo wako,Tabasamu lako Daima milele,Tulikupenda sana ila Mungu amekupenda zaidi,Pumzika kwa Amani Mzee wetu,” aliandika Joti.
Mzee Majuto ambaye alijizolea umaarufu mkubwa kwenye filamu alianza kuugua mwaka jana na mwaka huu serikali kwa kushirikana na wananchi walichanga pesa na kumpelekeka kwenye matibabu nchini India.
Muigizaji huyo alizaliwa mwaka 1948 jijini Tanga na kusoma shule Msambwini, Tanga, alianza kuigiza 1958 akiwa na umri wa miaka 9.
Taarifa za msiba huo wa nguli wa maigizo zimethibitishwa na Afisa habari wa Muhimbili Aminiel Eligaisha ambapo amesema Mzee Majuto amefariki akiwa anaendelea na matibabu ambayo aliyaanza Julai 31, mwaka huu baada ya jitihada za madaktari kuokoa uhai wake kushindikana.
''Hali yake ilibadilika majira ya saa tisa alasiri ya leo hivyo kuhamishwa kutoka jengo la  Sewahaji kwenda  ICU. Ilipofika saa 1.30 jioni hii hali yake ilibadilika zaidi na madaktari walijitahidi kuokoa maisha yale bila mafanikio. Ilipofika saa mbili alikata roho'', amesema.
Mzee Majuto alianza kuumwa muda mrefu akisumbuliwa na tatizo la nyonga ambapo mapema mwezi Mei alipelekwa nchini India kwaajili ya matibabu kabla ya kurejea nchini mwezi Juni ambapo alifikia Muhimbili lakini baadae alipata nafuu na kwenda nyumbani kabla ya kurudishwa tena Muhimbili baada ya hali yake kubadilika.
Mkongwe huyo alitangaza kustaafu kuigiza baada ya kutoka India lakini atakumbukwa kwa kazi zake nyingi za kuchekesha ambazo alizifanya kwa uhodari mkubwa na kuwavutiwa mashabiki wengi.
Marehemu Majuto alizaliwa mwaka 1948 mkoani Tanga na alianza maisha kwa kujishughulisha na shughuli za kilimo kabla ya kuingia kwenye sanaa ya maigizo ambayo ilimpatia umaarufu. Tutaendelea kukupatia taarifa na taratibu za mazishi na msiba kwa ujumla. Bwana alitoa Bwana ametwaa. Pumzika kwa amani mzee Majuto.

0 Comments

Previous Post Next Post