Wema Sepetu Abariki Diamond, Mobetto Kufunga Ndoa.

DAR ES SALAAM: Kwa mara ya kwanza, staa wa filamu Bongo, Wema Isaac Sepetu ametoa baraka zake kwa aliyekuwa mpenzi wake, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ amuoe Video Queen Hamisa Mobeto endapo watafikia uamuzi huo.

Kabla ya kufunguka hayo, Wema na Mobeto walikuwa hawaivi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kutokana na wawili hao ‘kubanjuka’ na Diamond kwa nyakati tofauti.

Akizungumza na Risasi Jumamosi, Jumatano iliyopita maeneo ya Kinondoni jijini Dar, Wema ambaye amelamba mashavu ya ubalozi kutoka Kampuni ya StarTimes na The Network ambayo ni kampuni mama inayoendesha Mchezo wa Namba wa Tatu Mzuka, alisema kuwa, hana kinyongo na Mobeto na Diamond hivyo wakikubaliana, waachwe waoane tu.

“Ni hivi watu huwa wanapenda sana kuunganisha matukio na ndiyo maana utaona usiku ule wa Tuzo za Sinema Zetu, walidai kwamba mimi nilionekana kukwazika baada ya Mobeto kumtaja Diamond kama mwanaume aliyemvutia kuliko wote pale ukumbini.

“Ninafikiri hawakujua tu kuwa hata wakati anamtaja na kuoneshwa kwenye zile skrini kubwa, mimi nilikuwa bize na simu ila nilishtuka baada ya watu kushangilia na sikujua hata kama kutakuwa na hisia za mimi kununa.

“Kiukweli watu wanatakiwa kufahamu wazi kuwa siku ile sikukasirika hata kidogo isipokuwa haya yote yanaunganishwa kwa kuwa kuna siku nilisema Diamond ni bosi wangu mpya pale Wasafi TV, hivyo wakadhani tumerudiana, lakini ukweli ni kwamba amebaki kuwa rafiki yangu na kaka yangu, upande mwingine ni bosi wangu tu.

“Pale Wasafi TV kuna kipindi ambacho tunakiandaa na mastaa wenzangu watatu ambacho tutakuwa tunakifanya, ingawa kwa sasa siwezi kuwataja hao wenzangu ambao nitakuwa nikifanya nao, ila kwa ufupi watu waamini tu wazi kuwa mimi na Diamond kwa sasa tupo kikazi zaidi na siyo mahaba tena.

“Siku zote nimekuwa nikijitahidi sana kusema kuwa Mobeto ni mdogo wangu sana tu na ninampenda na kumheshimu. Hivyo uhusiano wake na Diamond ninauona mzuri tu kwani tayari wameshakua mtu na mzazi mwenzake hivyo hata wakioana, mimi nitafurahi kwa sababu wanaendana na ‘couple’ yao inafurahisha sana kwa kweli,” alisema Wema.

TUJIKUMBUSHE KIDOGO

Wema ndiye mrembo wa kwanza kutokelezea na Diamond kwenye vyombo vya habari na kutengeneza ‘kapo’ iliyozungumzwa zaidi katika mitandao ya kijamii na mitaani.

Licha ya kapo yao kuzungumzwa na kupendwa na wengi, ilikuwa ikiwakata stimu mashabiki wa burudani baada ya kupitia vipindi vya kuachana na kurudiana kwa takriban mara mbili.

WEMA HAKUBAHATIKA MTOTO

Pamoja na kudumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu, Wema hakubahatika kuzaa na Diamond. Mkali huyo wa Bongo Fleva, alianza kupata baraka ya mtoto baada kukutana na Mganda, Zarinah Hassan ‘Zari The Lady Boss’.

Wakati Zari akiwa kwenye mahaba motomoto na Diamond hususan baada ya kumzalia ‘baby girl’ (Tiffah Dangote), Mobeto alikitia kitumbua mchanga kwa kubanjuka na Diamond kwa siri na kufanikiwa kubeba mimba iliyozua tafran kwa Zari.

UPEPO WAWEKWA SAWA

Hata hivyo, Mobeto alifanikiwa kumzalia Diamond mtoto wa kiume (Abdul), lakini Diamond alimwelewesha Zari na maisha yakaendelea kwa makubaliano kwamba, mpenzi wake atabaki kuwa Zari, kwa Mobeto atabaki kumlea mwanaye.

MARA PAAP! WAMWAGANA

Baadaye Diamond na Zari walimwagana, kitendo ambacho kinaelezwa kuwa ni fursa adhimu kwa Mobeto kushikilia mpini kwani tayari ni mzazi mwenziye.

Imeandikwa na Neema Adrian na Memorise Richard. 

0 Comments

Previous Post Next Post