Sakata la Kichapo cha Mama Diamond Kwa Hamisa Mobetto, Familia Yaingia Katika Vita Nzito.


Kama ni nyumba kushika moto, basi huu moto wa Madale ni wa gesi maana unaunguza hatari na mpaka sasa unaambiwa ‘faya’ hawana taarifa zozote kwani hakuna aliyepiga namba yao ya dharura 114 ili wafike eneo la tukio!

 Kitendo cha mama mzazi wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Sanura Kassim a.k.a Bi Sandra kumchezeshea kichapo kizito mwanamitindo Hamisa Mobeto a.k.a Tununu kimeipasua familia ya jamaa huyo kufuatia kuibuka kwa vita nzito.

 KABLA YA YOTE

Kabla ya yote, taarifa ikufikie kuwa, juzikati, Bi Sandra au mama Diamond alikiri kukutana uso kwa uso na Mobeto ndani ya nyumba kule Madale, nje kidogo ya Jiji la Dar na kumshushia kipigo hadi kumg’oa lile wigi lake kichwani.

Shukurani ziende kwa Diamond ambaye alimuokoa Mobeto kisha kumkimbizia kwenye gari na kumuondoa eneo la tukio, la sivyo, leo tungekuwa tunazungumza mengine huku kisa kikielezwa kuwa ni chuki tu, kwamba, mama huyo hampendi wala hamtambui kama mkwe wake aliyemzalia mwanaye mtoto wa kiume, Abdul.

Mara baada ya tukio hilo ndipo kulipoibuka mambo juu ya mambo ambapo vijembe vilianza kwenye mitandao ya kijamii.

DIAMOND Vs MAMA’KE

Taarifa za ndani ya familia hiyo zilidai kwamba, kitendo cha mama Diamond kumchapa Mobeto kilisababisha kuingia kwenye ugomvi mkubwa na

Diamond, jambo ambalo halikuwahi kutokea.


“Mara zote Diamond na mama yake wamekuwa ni zaidi ya mama na mwanaye kutokana na walivyokuwa wakipendana, lakini ghafla tu mambo yamebadilika kwa sababu ya Mobeto.

MOBETO ANATUMIA KIZIZI?

“Hapa ndipo nguvu ya mapenzi inapoonekana, yaani Diamond ambaye anajulikana anavyompenda mama yake, leo anabadilika na kuwa upande wa Mobeto? Kama ni kizizi, basi Mobeto ni noma!,” alidai mnyetishaji wetu ambaye aliomba hifadhi ya jina.

ZARI Vs MOBETO

Kufuatia tatizo hilo, mama Diamond aliingia kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuweka picha ya watoto wawili wa Diamond, Tiffah na Nillan aliozaa na Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ na kuwataka watu kufumba midomo kwa watoto hao wa Diamond.

Hata hivyo, muda mfupi baadaye, Diamond naye alitupia kwenye ukurasa wake wa Instagram picha ya mwanaye Abdul aliyezaa na Mobeto akiwa kwenye ngazi ya ghorofa tofauti na wale wa Zari kisha kusindikiza na maneno kuwa watoto wake ni wa maghorofani.

DIAMOND Vs MAMA’KE

Hapo sasa ndipo muziki ulipokolea ambapo kwa mujibu wa vyanzo vya ndani ya familia ya Diamond, kulitokea mpasuko wa aina yake huku vita hiyo ikiongozwa na mama Diamond na Diamond mwenyewe.

Ilidaiwa kuwa, mama Diamond hamtaki kabisa Mobeto aolewe na Diamond na badala yake bado mapenzi yake yapo kwa Zari ndiyo maana amekuwa akitupia picha za watoto wake huku akiwa hamtambui yule wa Mobeto.

QUEEN DARLEEN NA ESMA PLATNUMZ

Katika kunogesha vita hiyo, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa, hata dada zake Diamond, Mwanajuma Abdul ‘Queen Darleen’ na Esma Khan ‘Esma Platnumz’ nao wapo upande wa mama yao.

Queen Darleen alishanukuliwa mara kwa mara kuwa yeye anampenda Zari huku Esma akiweka wazi kuwa anampenda Wema Sepetu, lakini hamchukii Zari na wala hawezi kumpangia Diamond mwanamke wa kuwa naye.

Kwa maana hiyo, hesabu zinaonesha kuwa, Mobeto anakubaliwa na Diamond pekee, lakini mama yake na ndugu zake wengine wote wapo upande wa Zari hivyo siyo vita ya kitoto ambapo ilielezwa kuwa, baadaye baba huyo alimwondoa mwanaye huyo kwenye listi ya wafuasi (followers) wake wa Instagram.


KIKAO KIZITO

Habari zaidi zilieleza kuwa, wajomba na mama wadogo wa Diamond waliomba kuitisha kikao kizito cha kifamilia ili kuona namna ya kuliweka jambo hilo sawa kwani hawafurahiswi na kutoelewana kwa Diamond na mama yake.

BABA DIAMOND ACHACHAMAA

Katika mahojiano maalum na Risasi Jumamosi, baba mzazi wa Diamond, Abdul Jumaa alichachamaa kuonesha kuwa anachukizwa na malumbano hayo yanayoendelea ambapo mambo yalikuwa hivi;

Risasi Jumamosi:
Baba Diamond unazungumziaje suala la mzazi mwenzako, Bi Sandra kumpiga Mobeto ambaye ni mzazi mwenza wa Diamond?

Baba Diamond:
Dah! Kiukweli hakufanya kitu kizuri kabisa. Mimi mwenyewe sijapenda hata kidogo kwani yeye hapaswi kuingilia uhusiano wa watoto wala hapaswi kumchagulia mtoto mwanamke wa kuwa naye. Yeye angejisikiaje kama mama Hamisa angempiga Diamond? Kiukweli si picha nzuri hata kidogo.

Risasi Jumamosi:
Kwa sasa unawasiliana na Mobeto?

Baba Diamond:
Mmmh! Niliwasialiana naye kipindi kile cha 40 ya Abdul (mtoto ambaye Mobeto amezaa na Diamond), lakini tangu arudiane na Diamond, hakuna mawasiliano na mimi tena, sijui labla itakuwa ni ubize na majukumu kuwa mengi ndiyo maana hanikumbuki!

Risasi Jumamosi:
Je, ni mwanamke gani wa Diamond amewahi kuwa karibu na wewe na kukujali kama baba mkwe?

Baba Diamond:
Kwa kweli ni Wema Sepetu (naye aliwahi kuwa mpenzi wa Diamond). Alikuwa akinipenda sana, hata huku nyumbani kwangu (Magomeni, Dar) alikuwa anakuja na kumfanya Diamond kuwa karibu na mimi zaidi. Simaanishi wengine walikuwa hawanipendi, hapana, ila Wema alikuwa ananijali sana.

Risasi Jumamosi:
Asante, tutakutafuta siku nyingine.

Baba Diamond: Asanteni!

Source:GPL

0 Comments

Previous Post Next Post