Lulu Michael Kufanya Usafi Wizara ya Mambo Ndani.


JESHI la Magereza limemwachia msanii Elizabeth Kimemeta Michael, maarufu 'Lulu' aliyekuwa anatumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam, ili atumikie adhabu yake akiwa nje.

Akiwa nje, Lulu (22) amepangiwa kufanya kazi za huduma ya jamii katika viunga vya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, kwa mujibu wa amri ya Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam iliyoketi chini ya Jaji Ama-Isaria Munisi.

Jaji huyo alikubali Lulu kumalizia sehemu ya adhabu ya kifungo chake cha miaka miwili nje kwa kutumikia huduma za jamii ikiwamo kufanya usafi.

Mahakama Kuu ilifikia uamuzi huo baada ya Lulu kuwemo kwenye idadi ya wafungwa waliopewa msamaha wa Rais John Magufuli Aprili 26, mwaka huu pamoja na kukidhi vigezo vya maombi yake.

Kwa mujibu wa hati ya maombi yake yaliyowasilishwa mahakamani hapo, Lulu aliiomba sehemu yake ya kifungo iliyobaki katika miaka miwili aimalizie akiwa nje akitumikia huduma za jamii.

Novemba 13, mwaka jana Mahakama Kuu ilitoa adhabu ya kifungo cha miaka miwili jela kwa Lulu kwa kosa la kumuua bila kukusudia marehemu Steven Kanumba.

Kwa kuachiwa na Jeshi la Magereza mwishoni mwa wiki iliyopita, Lulu amekaa gerezani kwa siku 180 sawa na miezi sita badala ya 16 ambayo alistahili kutumikia kama asingepata msamaha wa Rais.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi hilo iliyotolewa na Kitengo cha Habari na Uhusiano jana, Lulu alichiwa Jumamosi iliyopita.

“Jeshi la Magereza Tanzania linaufahamisha umma kuwa mfungwa namba 1086/2017 Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka miwili katika gereza la Segerea jijini Dar es Salaam kwa kosa la kuua bila ya kukusudia ameachiliwa kutoka gerezani kwenda kutumikia kifungo cha nje,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Magereza, mfungwa yoyote isipokuwa mfungwa wa kunyongwa na wa maisha, mara baada ya kupokelewa gerezani hupata msamaha wa theluthi ya kifungo chake.

Ilieleza kuwa Lulu alipata msamaha huo na alitakiwa kuachiliwa huru Machi 12, mwakani.

Jeshi la Magereza lilifafanua kuwa Machi 26, mwaka huu katika kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, Rais Magufuli alitumia madaraka aliyopewa kikatiba kutoa msamaha robo ya adhabu kwa wafungwa wote waliokuwa na sifa za kunufaika na msamaha huo.

“Kufuatia msamaha huo mfungwa namba 1086/2017 Elizabeth Michael maarufu kwa jina la Lulu naye alinufaika na msamaha huo na hivyo kutakiwa kutoka gerezani Novemba 12, mwaka huu,” ilieleza zaidi taarifa hiyo.

“Mfungwa namba 1086/2017 Elizabeth Michael ameachiliwa Mei 12, mwaka huu na kwenda kutumikia kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania.”

Ilieleza kwa mujibu wa Seria ya Huduma kwa Jamii, wafungwa ambao vifungo vyao havizidi miaka mitatu hunufaika na utaratibu huo ambao unampa fursa mfungwa kutumikia kifungo chake nje ya gereza kwa kufanya kazi zisizo na malipo kwa manufaa ya jamii.

Ilifafanua kuwa Lulu kutokaa na kukidhi vigezo vya kisheria na kuonesha tabia njema akiwa gerezani amenufaika na utaratibu huo.

MARA YA KWANZALulu alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, Aprili 12, 2012 kwa mauaji ya Kanumba.

Katika kesi ya msingi ilidaiwa kuwa Aprili 7, 2012 Lulu alimuua Kanumba bila kukusudia.

Akisoma hukumu Novemba 13, mwaka jana, Jaji Rumanyika alisema mahakama yake imepitia ushahidi wa Jamhuri na kujiridhisha bila kuacha shaka kuwa umethibitisha makosa dhidi ya mshtakiwa na kwamba hata katika utetezi wake mshtakiwa amejikanganya.

Alisema mshtakiwa alisema Kanumba alikuwa amelewa lakini wakati huohuo aliweza kukimbia umbali wa hatua 27 na nusu bila kuanguka na kufanikiwa kumkamata, kumburuza na kumwingiza ndani.

Jaji Rumayika alisema pia Lulu alikiri kwamba ni mtu pekee aliyekuwa na marehemu kwa mara ya mwisho lakini katika utetezi wake hakusema nini hasa kilitokea hadi aliyekua mpenzi wake huyo akakutwa na mauti.

Jaji Rumanyika alisema mshtakiwa aliieleza mahakama kwamba alikuwa kwenye mahusiano na mshtakiwa kwa miezi minne, alifahamu kuwa alikuwa na wivu wa kupitiliza hivyo hakutakiwa kupokea simu hiyo iliyosababisha ugomvi wao.

"Kwa mujibu wa kifungu cha 195 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, namtia hatiani mshtakiwa dhidi ya mauaji ya bila kukusudia," alisema Jaji Rumanyika.

"Utakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka miwili." 

0 Comments

Previous Post Next Post