Baby J Afunguka Kilichomfanya Kuwa Kimya Kwenye Game.

Baby J Afunguka Kilichomfanya Kuwa Kimya Kwenye Game

WASWAHILI tuna msemo unasema, kila zama na mvua zake si, ndiyo? Sasa zama fulani hivi za nyuma, mwishoni kwa miaka ya 2000, mwanadada kutoka Zanzibar, anayejulikana zaidi kwa jina la Baby J alikuwa ni miongoni mwa mvua kwenye gemu la Muziki wa Bongo Fleva.

Wengi watakumbuka ngoma zake nzuri za kuimbika na zenye maudhui ya mahaba. Zaidi zinaweza kuwa zinawakumbusha baadhi ya watu wakati ‘zinahiti’ walikuwa wanaziimba na kina nani!

Ngoja nikukumbushe chache. Unakumbuka ngoma ya Bwashee Bwashee ambayo mwanadada huyu aliimba na Ali Kiba? Vipi kuhusu Moyo Wangu alioimba na Pasha? Mpenzi Wangu je alioimba na Banana Zorro unaukumbuka? Huu hata mimi ninaupenda zaidi!

Ukweli ni kwamba mwanadada huyu aliuteka muziki na alikuwa anafanya vizuri kwa nyimbo tamu. Lakini kwa sasa hatumsikii tena, kiufupi kapotea na bila shaka wengi wangependa kufahamu ni wapi alipo na anafanya nini? Si ndiyo?

Haya huyu hapa Risasi limekuletea.

Risasi: Baby J mambo vipi, umepotelea wapi?

Baby J: Mbona nipo jamani.

Risasi: Tunafahamu upo lakini kimuziki hatukusikii kabisa.

Baby J: Ni kweli nilikuwa nimepotea kidogo kutokana na mambo ya maisha ya hapa na pale lakini hivi karibuni narudi maana nimefanya kazi na MwanaFA, ninatarajia kuiachia baada ya mfungo unaokwenda kuanza ‘soon.’


Risasi: Kabla ya kuzungumzia ujio wako huo mpya, hebu tuzungumzie kilichokupoteza ni nini hasa, hayo mambo ya maisha ndiyo yapi?

Baby J: Ni mambo ya maisha tu ambayo sidhani kama naweza kuweka wazi, lakini inaweza kumtokea mtu yeyote yule akarudi nyuma, si unajua tena maisha.

Risasi: Au uliolewa?

Baby J: Hahahaa (anacheka), hapana. Sijaolewa jamani, ni mambo tu ya maisha ya hapa na pale, niseme tu changamoto za kimuziki na maisha mengine ya nje ya muziki.

Risasi: Kwa hiyo kwa sasa vyote hivyo vimekwisha ndiyo maana unarudi kwenye gemu upya?

Baby J: Yah! Kwa kiasi kikubwa baadhi ya mambo nimeshayaweka sawa na ndiyo maana nimeamua kurudi.

Risasi: Kwani huko Zanzibar zaidi unajishughulisha na nini hasa mbali na muziki?

Baby J: Kwanza huku ni nyumbani. Lakini pia kuna biashara zangu ambazo nashughulika nazo na mambo mengine ya kimaisha.

Risasi: Biashara gani hizo unafanya?

Baby J: Hahahaaa (anacheka tena), za kawaida tu. Si unajua maisha ni kupambana.

Risasi: Unaonekana wewe ni msiri sana, haya bwana. Lakini nini unamisi kwenye ‘mainstream’?

Baby J: Kiukweli ile kutrend kwenye media mara kwa mara lakini pia kampani kutoka kwa wasanii wenzangu. Unajua kampani ya wasanii si kama ya watu wa kawaida. Kuna vingi mnakuwa mnashare.

Risasi: Hummis mpenzi wako ambaye kwa sasa ni mwanamuziki mkubwa?

Baby J: Hahahaaa (anacheka), nani huyo?

Risasi: Kwani hujawahi kutoka na staa?

Baby J: Niliwahi kutoka naye lakini wengi hawamfahamu na siwezi kumuweka wazi.

Risasi: Kwa nini?

Baby J: Aaaa nikimtaja kwa sasa itakuwa balaa.

Risasi: Au ni huyu aliyeoa hivi karibuni na hutaki kuvunja ndoa yake?

Baby J: Hahahaaa (anacheka), kiukweli sifahamu na sihitaji kulizungumzia hili zaidi.

Risasi: Haya basi zungumzia ujio wako zaidi, kwa nini umeamua kurudi na MwanaFA?

Baby J: Kwa sababu ni mwanamuziki mzuri na wimbo ulikuwa unamhitaji yeye. Lakini jambo lingine ni kwamba nimekaa kimya muda mrefu kwa hiyo kwa kurudi na MwanaFA ambaye ni mwanamuziki mwenye heshima na ana mashabiki wengi kwangu nahisi ni jambo zuri.

Risasi: Asante sana Baby J, bila shaka mashabiki wako angalau wamefahamu upo wapi kwa sasa.

Baby J: Asante sana na kwa mashabiki wangu, kiukweli nawapenda na tupo pamoja. 

0 Comments

Previous Post Next Post