Aunt Ezekieli Kuigawa Bure Filamu yake Mpya.


Mwigizaji wa filamu, Aunty Ezekiel amesema anakusudia kuwagawia bure filamu yake mpya Mama ni Mungu wa Dunia atakayoizindua Mei 13 mwaka huu, wageni wote watakaofika siku hiyo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Aunty amesema lengo la kufanya hivyo ni kuwafikishia ujumbe alioukusudia watu wengi ziadi.

Amesema alipata wazo la kuufikisha ujumbe uliobebwa katika filamu hiyo baada ya kuwa mama. Aunty ni mama wa mtoto mmoja wa kike aitwaye Cookie.

“Nilipoingia leba niliona mateso ambayo wanawake wanapitia katika kupata mtoto nikaona hamna shukrani nyingine ambayo naweza kuitoa kwa mama zaidi ya kutengeneza filamu,” anasema.

Pia, amesema maisha ya kutokuwa na mama yalimuongezea ari ya kutaka kutengeneza filamu hiyo kwa mama yake ambaye alifariki wakati yeye akiwa na miaka minane tu.

“Yaani pamoja na kwamba sasa hivi ni mama, kuna wakati unakumbana na mambo mazito ambayo unatamani mama yako angekuwepo ili umshirikishe lakini ndio hivyo haiwezekani, hivyo filamu hii inatoa mafunzo kwa watu kuona thamani ya mama', amesema.

Akielezea sababu ya kumshirikisha mtoto wake, amesema ni katika kuleta uhalisia zaidi na aliamini kuwa itampa hisia zaidi wakati wa kuigiza tofauti na ambavyo angecheza na mtoto asiye wake.

Filamu hiyo itazinduliwa Mei 13 mwaka huu katika Ukumbi wa Mlimani City na kwamba hana mpango wa kuisambaza zaidi ya watu kuionea kwenye mtandao wa Youtube.

0 Comments

Previous Post Next Post